Kulikuwa na binti mmoja aliyeishi maisha ya peke yake kwenye chumba kimoja alichokuwa amepanga. Alikuwa binti mdogo aliyeanza kuishi maisha hayo baada ya kumaliza chuo, lakini hakupata kazi wala mpenzi wa kumuoa. Maisha yake ya mahusiano hayakuwa mazuri, maana alikuwa ametendwa mara nyingi mpaka kufikia hapo.
Kwenye upande wa kazi, alikuwa anafanya kazi ya kuuza duka ambalo halikuwa lake. Yaani, yeye alikuwa mtu anayekwenda kuuza duka asubuhi na kurudi usiku, lakini duka na vilivyomo vilikuwa si vyake. Kupitia kazi hiyo ya kuuza duka, alikuwa akipata pesa kidogo ya kulipa chumba anachoishi na chakula cha kawaida.
Kila mara mwanamke huyo alionekana kutoamini wanaume, kiasi cha kuchukia kuwa nao kabisa. Hii ilitokana na mahusiano kadhaa aliyopitia na kuvunjwa moyo huko nyuma. Wanaume wengi waliokuwa wanahitaji kuwa naye hawakupata nafasi, na hata waliopata, waliishia kuachwa kila alipokumbuka jinsi wanaume walivyomuumiza kwenye mahusiano ya nyuma. Hii ilimfanya mara nyingi awe anatembea peke yake. Alikuwa haongozani na mtu anapotoka kazini kwake au kurudi. Kulikuwa na umbali kiasi kutoka anapouzia duka hadi kwake, lakini alikuwa anatembea kwa miguu kwa sababu umbali haukumchosha. Hata hivyo, katika kutembea kwake, changamoto kubwa aliyokuwa anakutana nayo ilikuwa ni mbwa.
Mbwa walikuwa wengi njiani alipokuwa akirudi kwake, hasa akichelewa usiku. Pamoja na kupita mara nyingi, alikuwa anaogopa sana mbwa. Tangu utotoni, alikuwa mtu anayewaogopa sana mbwa na kuwachukia, kwa sababu mbwa wa jirani yao alimng’ata akiwa na umri wa miaka 8. Tukio hilo lilimfanya aogope sana mbwa katika maisha yake yote.
Siku moja, katika njia ya kurudi nyumbani, alikutana na mbwa mmoja mdogo. Mbwa huyo alikuwa mbele yake, na alipomuona tu, alipunguza mwendo ili wapishane kwa tahadhari. Wakati wakipishana, mbwa akabweka ghafla, “Wouh!” Yule dada akaanza kukimbia kuelekea kwake. Mbwa kuona hivyo, akaanza kumkimbiza mpaka akaanguka chini baada ya hatua chache huku mbwa akiwa nyuma yake.
Baada ya kuanguka, mbwa alifika pale alipokuwa yule dada, lakini hakufanya chochote zaidi ya kumnusa na kuanza kurudi nyuma. Dada alipomuona mbwa anarudi, alinyanyuka haraka na kuendelea na safari ya kurudi nyumbani kwa haraka, akitembea huku akijipangusa vumbi kwenye nguo na kuangalia kama bado anafuatwa. Mbwa alibaki kusimama mbali, akimuangalia kwa umbali.
Baada ya hatua nyingi za kutembea, yule dada aliangalia nyuma na kukuta mbwa yule anamfuata taratibu. Hilo lilimshangaza sana, likamfanya aongeze mwendo mpaka akafika nyumbani bila matatizo, ingawa nguo zake zilikuwa zimechafuka kwa vumbi. Ilikuwa kawaida kwake kukimbizwa na mbwa, hivyo hakuchukulia kama jambo kubwa sana.
Lakini baada ya siku hiyo, alianza kushangazwa na jambo ambalo halijawahi kumtokea maishani. Mbwa yule alianza kumfuata kila mara na kujipitisha karibu na nyumbani kwake. Kila alipokuwa akitoka au kurudi, alikuwa akimuona mbwa huyo akiwa karibu naye au akimfuatilia kwa umbali.
Hili lilikuwa jambo geni kwake, maana hajawahi kuwa na urafiki na mbwa. Wakati mwingine alikuwa akimtupia mawe, lakini mbwa hakuwahi kuacha kumfuata kwa upole uleule. Alijaribu kumfanyia ubaya mara kadhaa, lakini mbwa hakukoma kuhitaji kuwa karibu naye. Wakati mwingine alikuta amelala mlangoni kwake.
Baada ya matukio mengi, yule dada aliamua kuanza kumchukulia yule mbwa kama mbwa wake. Ingawa hakuwahi kufanya hivyo maishani mwake, aliamua kujaribu tu kumfuga. Alianza kumjali kwa kumpa chakula, hadi wakaanza kutembea pamoja kwenye baadhi ya safari zake. Alishangazwa sana na jinsi mbwa huyo alivyokuwa mwaminifu kwake, hasa alipokuwa anarudi nyumbani usiku. Alikuwa akitembea naye kwenye njia alizokuwa akiziogopa bila uoga. Mbali na hilo, alianza kukosa hofu hata alipokutana na mbwa wengine, maana sasa alikuwa ameelewa tabia zao kupitia mbwa wake.
Mwisho wa yote, hakujutia kabisa kumfuga mbwa huyo, ingawa baada ya mwaka mmoja alikufa kwa kugongwa na gari akiwa kwenye mizunguko yake. Lakini aliacha funzo kubwa kwa yule dada juu ya kutoa nafasi ya upendo kwa watu au vitu anavyoviogopa, kwa sababu hajavijua vizuri. Alifanikiwa mpaka kupata mtu anaempenda sana na kuishi nae kwa uaminifu maishani.
Kutokana na mambo aliopitia, Kila mara alikua akishuhudia watu kuwa kuna wanawake hupitia mahusiano kadhaa yanayovunja moyo, kiasi cha kufanya wasihitaji ukaribu wa mapenzi ya kweli kwa wanaume. Wengine hawapiti huko, lakini kutokana na matukio au simulizi mbalimbali, wanashindwa kuamini wanaume. Kuna ambao husema hata “Wanaume wote ni mbwa,” na kuzingatia pesa. Wanafanya hayo wakisahau kwamba hata huyo Mbwa anaweza kuwa wao, akawapenda, kuwafurahisha, na kuwalinda Kila siku. Kikubwa ni uwe tayari kumpa nafasi, huku na yeye akiwa tayari kuwa wako.
Mukijua mambo haya hamuwezi kuachana na Mpenzi wako kirahisi BONYEZA HAPA>>>



