SIRI NA SHEMEJI (Simulizi fupi ya Kusoma)

Anisa alikuwa mwanamke mzuri, mwenye heshima na upendo kwa mume wake, Kevin. Ndoa yao ilikuwa changa, yenye matumaini makubwa na ndoto za baadaye. Hata hivyo, nyuma ya tabasamu zake za kila siku, Anisa alikuwa anabeba siri nzito.

Muda mrefu uliopita kabla ya kuolewa na Kevin, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na rafiki wa karibu sana wa mume wake aitwaye Marcus. Uhusiano huo ulivunjika kutokana Marcus kumuacha Anisa. Anisa alipoamua kuwa Kevin ndiye mwanaume wa maisha yake, Marcus alitambuliswa na Kelvin kuwa ameoa mwanamke aitwae “Anisa” na ndio atakua Shemeji yake. Marcus alikubari swala hilo na wala hakutaka kuuongelea uhusiano wake na Anisa kwa Kelvin. Lakini moyoni, Marcus hakuwa tayari kuachilia uhusiano wao wa zamani na Anisa. Alianza kumtafuta tena Anisa kwa njia za siri, akimtumia jumbe za kimapenzi kila mara, na kumfanya asiwe na amani.

Anisa hakutaka kumuumiza mume wake wala kuharibu urafiki wa Kevin na Marcus, hivyo aliamua kubeba mzigo huo kimya kimya. Kila wakati alipokea jumbe za Marcus, alifuta haraka, akijaribu kusahau na kuishi kama hakuna kilichokuwa kikiendelea. Lakini usumbufu huo ulianza kumkosesha amani na kumfanya kuwa na mawazo mengi.

Kevin aliona mabadiliko hayo kwa mke wake. Alianza kuhisi kuwa Anisa anaficha kitu. Tabasamu lake lilikuwa la bandia, na mara nyingi alikuwa kwenye mawazo. Moyo wa Kevin ulianza kumshuku mke wake. Alihisi kuwa huenda Anisa alikuwa anamficha jambo zito. Ili kupata ukweli, aliamua kuchunguza simu ya mke wake bila ridhaa yake.

Alishika simu ya Anisa wakati alipokuwa amelala, akafungua meseji. Ndani ya meseji hizo, aliona maneno ya kimapenzi kutoka kwa rafiki yake wa karibu, Marcus. Kevin alichanganyikiwa. Bila kujiuliza mara mbili, aliamini kuwa Anisa alikuwa amemsaliti kwakua na mahusiano ya mapenzi na rafiki yake wa karibu.

Hasira na huzuni zilimjaa Kevin na alimwambia mkewe kuhusu jambo alilolikuta kwenye simu yake. Hakutaka kusikiliza chochote maana mawazo ya kifo yalimwingia kichwani. Hakuwa na nguvu za kuongea na Anisa wala kwenda kukabiliana na rafiki yake.
Bila kumkabili Anisa au kujaribu kuelewa zaidi, aliondoka nyumbani akiwa amejaa maumivu, akitembea kwa hasira barabarani.

Alifika kwenye barabara yenye magari mengi, moyo wake ukiwa umevunjika kabisa. Alitamani maumivu hayo yaishie haraka, na hakuhisi tena thamani ya kuendelea kuishi. Ghafla, gari lilikuja kwa kasi na kumgonga Kevin, likamrusha pembeni.

Anisa, akiwa ndani ya nyumba, alihisi kuna jambo baya lililokuwa limetokea. Aliposhindwa kumtafuta Kevin kwa simu, moyo wake ulijawa na hofu. Baada ya muda, alipokea simu kutoka hospitali: “Mume wako amepata ajali mbaya, anahitaji matibabu ya haraka.”

Anisa alikimbilia hospitali, machozi yakimtiririka, moyo wake ukiwa umejaa wasiwasi. Alipofika, aliambiwa kwamba Kevin alikuwa hajafa, lakini alikuwa katika hali mbaya sana, hawezi kuzungumza, wala kuutikisa mwili wake. Ajali ile ilimwacha na majeraha ya ndani yaliyoathiri uwezo wake wa kufanya mambo.

Anisa alilia kwa uchungu, akijilaumu kwa kilichotokea. Alijua tu kuwa Kevin alikuwa kwenye hali hiyo kwa sababu ya tukio la kuona Jumbe za Marcus kwenye simu yake. Alijaribu kumjulisha hayo Marcus kuhusu ajali hiyo na kile kilichosababisha Kevin apate ajali. Marcus, aligopa sana jambo hilo, aliamua kukimbia mji haraka, akiacha kila kitu alichokua akifanya. Hakutaka kukabiliana na matokeo ya vitendo vyake.

Siku zilibadilika kuwa wiki, na wiki zikawa miezi. Anisa hakukata tamaa. Aliendelea kumtunza Kevin, akihakikisha anapata huduma bora zaidi hospitalini. Kila siku, alikuwa pale akimshika mkono, akimuombea apone na kurudi kuwa yule mume aliyempenda. Ingawa Kevin hakuweza kusema wala kutikisa mwili wake, macho yake yalimuonyesha mazuri yote aliokua anafanya Anisa kwa wakati huo.

Baada ya miezi mitatu ya mapambano ya kiafya ya muda mrefu, Kevin alianza kuonyesha dalili za kupona. Polepole, alianza kupata nguvu za kuzungumza na kutikisa mwili wake tena. Aliona upendo ambao hakuutarajia kutoka kwa Anisa, aliyeendelea kumhudumia licha ya hali ngumu waliyopitia. Kila siku, Anisa alimwomba msamaha kwa kile kilichosababisha maumivu yote hayo, akimweleza ukweli kuhusu Marcus na jinsi alivyojaribu kutaka awe nae bila mafanikio.

Kevin, akiwa sasa na akili iliyotulia na moyo uliopata nafuu, alitafakari upendo wa Anisa na kujitolea kwake. Ingawa aliumizwa na yaliyotokea, aliweza kuona kuwa Anisa hakumsaliti ila alikuamejaribu kumlinda kwa Siri tu. Aliamua kumsamehe mke wake, akifahamu kuwa mapenzi yao yalikuwa na nguvu ya kustahimili dhoruba hiyo nzito.

Mwisho, walirudi nyumbani pamoja wakiwa na upendo zaidi ya sana. Waliahidi kutokuwa na siri tena, wakifahamu kwamba kusikilizana na uaminifu ndiyo msingi wa ndoa yao.

Umejifunza nini kupitia simulizi hii? Endelea kuwa karibu na The bestgalaxy.

2 thoughts on “SIRI NA SHEMEJI (Simulizi fupi ya Kusoma)”

Leave a comment