Kusafiri kwa gari kunaweza kuwa furaha au mateso kulingana na jinsi mwili wako unavyokabiliana na mwendo. Kwa baadhi ya watu, changamoto kubwa ni motion sickness; hali ya kichefuchefu kinachosababishwa na ubongo kuchanganyikiwa kutokana na taarifa tofauti kutoka kwenye macho na masikio kuhusu mwendo. Kuna wengine tatizo hili huanza hata kukusikia harufu flani ndani ya gari.
Kutapika ukiwa kwenye gari kunaweza kukukuta kutokana na kichefuchefu hiki. Lakini uzuri ni kwamba unaweza kupunguza au kuondoa kabisa kichefuchefu ukiwa safarini. Hapa chini kuna njia zenye maelezo ya kutosha unazoweza kutumia ili kufanya hivyo.
Ujumbe mzuri wa kumtumia mpenzi wako kwa sms BONYEZA HAPA>>>
Njia za kuzuia kichefuchefu au kutapika kwenye gari
1. Kaa Sehemu Sahihi
Kiti cha mbele ni rafiki yako. Ukiwa kwenye kiti hicho, mwili wako hupata mtikisiko mdogo ukilinganisha na viti vya nyuma, na unaweza kuona barabara kwa uwazi zaidi. Hii inarahisisha ubongo wako kulinganisha mwendo unaouona na ule unaouhisi, hivyo kupunguza kichefuchefu.
2. Tazama Mbele, Si Pembeni
Kuangalia mbele husaidia ubongo wako kuelewa vizuri mwendo wa gari. Ukigeuka mara kwa mara pembeni au nyuma, macho yako yatatuma taarifa zinazokinzana na hisia za mwili, na matokeo yake ni kichefuchefu.
3. Pata Hewa Safi
Hewa yenye joto kali au harufu mbaya inaweza kuongeza kichefuchefu. Fungua dirisha kidogo ili upepo baridi uingie, au washa kiyoyozi. Ikiwa kuna harufu ya mafuta, vyakula vizito, au manukato makali ndani ya gari, jaribu kuiepuka kwa kugeuza uso au kukaa karibu na chanzo cha hewa safi.
4. Kula Mlo Mwepesi Kabla ya Safari
Kula chakula kizito kabla ya safari ni kama kualika matatizo. Vyakula vya mafuta, vya kukaanga au vyenye harufu kali huongeza uwezekano wa kutapika. Badala yake, kula vyakula vidogo na vyepesi kama biskuti kavu, mkate, au matunda yasiyo na tindikali nyingi. Lengo ni kuhakikisha tumbo haliko tupu kabisa, lakini pia halijazidiwa.
5. Jaribu Tangawizi au Peppermint
Tangawizi ni tiba ya asili inayojulikana kupunguza kichefuchefu. Unaweza kunywa chai ya tangawizi, kutafuna biskuti yenye tangawizi, au kutumia pipi ya tangawizi. Peppermint pia husaidia kwa kutuliza misuli ya tumbo na kupunguza hisia za kutapika. Weka pipi ndogo mfukoni kabla ya safari.
6. Fanya Mapumziko
Kama safari ni ndefu, kuendelea kukaa kwenye gari kwa muda mrefu huongeza dalili za motion sickness. Simama kila baada ya saa 1-2, tembea kidogo, pumua hewa safi, na nyoosha miguu. Hii itasaidia mwili wako kupata mwendelezo mpya wa hisia na kupunguza kizunguzungu.

7. Epuka Pombe na Kafeini Nyingi
Pombe inaweza kusababisha upungufu wa maji mwilini na kuathiri usawa wa mwili, huku kafeini nyingi ikiongeza wasiwasi na mapigo ya moyo. Yote haya yanaweza kuchochea kichefuchefu. Ni vema kunywa maji ya kawaida au juisi nyepesi badala yake.
8. Tumia Dawa za Kuzuia Motion Sickness
Kwa watu wanaopata tatizo hili mara kwa mara, dawa maalum kama Dramamine, Avomine, au Bonamine zinaweza kusaidia. Ni vizuri kutumia dawa hizi dakika 30 hadi saa 1 kabla ya safari. Kumbuka, tumia dawa baada ya ushauri wa daktari au mfamasia, hasa kama unatumia dawa zingine.
Mwisho; Kama dalili zimeanza, jaribu kupumua kwa utaratibu kupitia pua, kisha utoe pumzi taratibu kwa mdomo. Weka macho yako kwenye kitu kisichohama mbele yako, na epuka kufumba macho kabisa. Njia hii inaweza kuzuia kutapika ndani ya dakika chache bila dawa.