Kwenye mahusiano, karibu watu wote huwa wanasema maneno ya kuaminisha kama “wanakupenda” na “upo peke yako,” lakini sio kila mtu humaanisha. Baadhi ya watu wanaweza kusema “Nakupenda” au “Upo peke yako,” lakini wakawa na wapenzi wengi wanaowaambia hivyo kila siku. Mtu muaminifu akiingia kwenye mahusiano na watu wa namna hii, kuna hatari kubwa ya kupata hata magonjwa ya moyo kwa mshtuko. Ukiacha mishtuko, mawazo pia huwa hayapingiki mnapoendelea kuwa pamoja.
Lakini uzuri ni kwamba kuna namna ya kujua mtu ambaye ana wapenzi wengi. Njia hii ni ya kuangalia ishara kwenye matendo yake na sio maneno yake. Kwenye makala hii naenda kuzungumzia ishara hizi, ila ni kwa upande wa mwanaume. Kwa hiyo kama unahitaji kujua ishara za mwanaume kuwa na wanawake wengi, basi hapa ni sehemu sahihi.
Maswali ya kumuuliza mpenzi wako mpya BONYEZA HAPA>>>
Ishara 5 za Mwanaume Kuwa na Wanawake Wengi
1. Simu yake na yaliomo ni siri
Simu yake inaweza kuwa inalindwa kama imeficha siri ambayo hautakiwi kuijua kabisa. Anaweza kuwa hawezi kukupa uitumie, na hata akikupa, haupati uhuru. Hii inaweza kuwa ni kwasababu ya kuficha mambo yanayoendelea kuhusu wanawake wengine.
Kuna wakati mtu anaweza kuwa hataki simu yake iwe mikononi mwa mtu mwingine kwa sababu tofauti na hiyo, lakini wanaume wasiotulia kwenye mahusiano huwa wanakuwa hivi pia ili kuficha wanayofanya.
2. Hakupi muda wa uhakika
Mwanaume mwenye wanawake wengi huwa hatabiriki kwenye suala la kukupa muda wa kuwa naye. Anaweza kuwa anatumia muda mdogo sana na wewe, na muda huo si wa uhakika. Muda mwingi husema yupo “busy” na hataki umfuate sehemu kukutana naye bila taarifa.
Wengine huwa wanakutafuta wanapokutana na hitaji la kimwili tu. Hapo ndio wanakupa muda sana na wakifanikisha wanachokitaka kutoka kwako, hurudi kwenye hali ya kutokua na muda.
3. Haongelei maisha yake wala muelekeo wenu
Mnaweza kuongea vitu vingi vya kufurahisha na mwanaume huyu, lakini hauwezi kugusa kuongelea maisha yake sana au maisha yenu ya baadaye. Wengine huwa maongezi yao makubwa ni starehe na kukutana kimwili.
Kiufupi, hataki umjue sana na hata ukimjua, hataki kukupa matumaini ya kuwa utakuwa naye kwa muda mrefu. Anakua kwenye mahusiano lakini haingii sana ndani maana yupo na wanawake wengi kwenye mahusiano.
4. Hujionesha lakini bila wewe
Mwanaume mwenye wanawake wengi anaweza kuwa na tabia ya kutotaka kuonekana na wewe sana kwenye maisha ya mitandao au maisha halisi. Kutokana na watu kutumia zaidi mitandao ya kijamii, basi naweza kusema upande wa mitandao ya kijamii ndio wa kuzingatia zaidi.
Mwanaume huyu huwa hawezi kuonesha picha ambayo inaonesha kujihusisha nawe. Hii inaweza kuwa ni kwa sababu anaogopa kuwashtua wanawake wengine aliowakamata.
5. Hana wivu wa kweli
Mwanaume mwenye wanawake wengi huwa hana wivu wa kweli pale anapokuona upo na wanaume wengine. Yaani, akiona umeanza kuonesha tabia ya kumsaliti, huwa haumsumbui kichwa kabisa. Anaweza hata kujua kabisa una mwanaume mwingine lakini asichukulie kama ni kitu kikubwa sana kiasi cha kuvunja mahusiano.
Kiufupi, wanakuwa kama ni wavumilivu sana kwenye mahusiano hata ukiwafanyia vitu vikubwa, lakini ukweli ni kwamba hawana wivu.
Uzuri wa hizo ishara 5 za mwanaume kuwa na wanawake wengi ni kwamba unaweza kuziangalia hata kwenye mahusiano machanga. Baadhi ya wanaume wenye wapenzi wengi huwa hawawezi kuzificha kabisa. Ndani ya mwezi mmoja tu katika mahusiano, unaweza kugundua ishara 2 au mpaka 4.