Baada ya kuzisoma simulizi tatu nzuri; Sukari ya Dada, Utamu wa Jumla na Mzigo wa Wakubwa, nimegundua funzo kubwa kuhusu maisha halisi ambalo hapa nitaweka wazi.
Simulizi hizi tatu ni miongoni mwa simulizi nzuri sana ambazo zimesimulia maisha ya watu tofauti wanaoishi katika ulimwengu mmoja.
Kila simulizi lina hadithi yake tofauti, lakini unaposoma zote kwa pamoja, unagundua zinaunda picha moja kubwa inayogusa maisha ya vijana, mapenzi, na changamoto nyingine katika jamii.
Baada ya kuzisoma kwa makini, haya ndiyo mambo matatu kati ya mengi muhimu niliyojifunza;
Mambo 3 Niliojifunza Baada ya Kusoma simulizi
1. Usifanye Usichopenda Kufanyiwa
Hili limejitokeza sana katika simulizi ya Mzigo wa Wakubwa.
Mhusika mkuu alijikuta akimfanyia rafiki yake jambo baya; kuchukua pesa zake ili kuokoa hali yake binafsi. Lakini muda haukupita, naye akajikuta akifanyiwa jambo lilelile na mtu mwingine wa karibu sana.
Maumivu aliyoyapata yalikuwa makubwa, lakini hakuweza kulalamika kwa sababu alitambua kwamba naye aliwahi kufanya kosa hilo.
Hapa kuna somo moja kubwa:
“Ukifanya ubaya, ujue ipo siku utaukuta uso kwa uso… Inaweza kuwa si leo, lakini ipo siku.”
2. Huwezi Kumpima Mtu kwa Kuangalia Tu
Hili nimejifunza kupitia simulizi mbili; Sukari ya Dada na Utamu wa Jumla.
Mwisho wa Sukari ya Dada, muhusika mkuu anakutana na Tausi na kuhisi kuwa anaishi na virusi vya UKIMWI.
Lakini unaposoma Utamu wa Jumla, unakuja kugundua kuwa Tausi hana virusi kabisa!
Hii imenifunza kitu kimoja muhimu sana:
“Usihukumu mtu kwa muonekano wake wa nje au mazingira yake. Ni ngumu kujua hata vita gani anaipigana ndani yake.”
3. Kila Mtu Ana Njia Yake ya Mafanikio
Katika simulizi zote tatu, wahusika walionesha njia tofauti za kupambana na maisha.
Wote walikuwa vijana waliokataa kukata tamaa. Yani kila mmoja alipambana kwa namna yake hadi kufikia mafanikio ambayo anayahitaji. Hakuna aliekubali kushindwa, wote walikubali kusonga mbele kutafuta ushindi kwenye njia zao.
Simulizi hizi zimenikumbusha kuwa:
“Hakuna njia moja sahihi ya kufanikiwa. Kila mtu ana wakati wake, njia yake, na changamoto zake za kipekee.”
Kwa ujumla, simulizi hizi tatu zimebeba uhalisia wa maisha ya sasa kwa upande wa vijana. Kwaiyo nilioyaongelea tu, utaona zinatuonesha kuwa dunia ni duara unachokifanya leo, kinaweza kukurudia kesho. Zinatusukuma pia kuwa waangalifu, wenye huruma, na wenye subira katika safari zetu za mafanikio.
