Nilikua nimeolewa na ninaishi na mume wangu kwa amani sana. Katika miaka yetu michache ya ndoa, kulikua na changamoto moja tuliyopitia na siwezi sema wazi niliimaliza vipi sasaivi, lakini acha nifafanue mambo yalivyokua.
Mme wangu alikua na rafiki yake mmoja anaitwa Mambe; Aliekua kama ndugu kwake. Kabla ya mume wangu kukutana na mimi, alikua na huyo rafiki yake, hivyo mimi ndio nilikua mgeni kwenye urafiki wao.
Urafiki wao haukua wa kuitana rafiki tu, walikua wameungana pamoja hata kwenye kazi. Walikua wanafanya kazi sehemu moja na wanashirikiana kwenye mambo mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi.
Huko kazini, nilikua nasikia huyu rafiki ndio mwenye cheo kikubwa na pia anaundugu na bosi wao mkubwa kabisa. Mme wangu alikua ananisimulia mambo mengi mazuri anayofanya huyo rafiki yake. Alikua anasema “Huyu Mambe ni ndugu yangu” kila mara tunapomuongelea.
Na ukweli huyo rafiki yake alikua anaonekana mstaarabu sana, lakini siku moja kwenye kupiga stori na mmoja wa marafiki zangu alinieleza mambo ambayo sikuamini kuhusu yeye. Huyu rafiki yangu alikua anaitwa Lisah na alikua ananisuka nywele huku akinipa stori za huyo mwanaume.
Nakumbuka alisema huyo Mambe ni mwanaume mpole, anaishi peke yake, lakini anawanawake wengi sana hapo mjini anao wahudumia na hawajijui. Ilikua ni kawaida sana kusema watu tukiwa na rafiki yangu, maana ni mtu anayejihusisha na kusuka nywele huku akiongea sana. Lisah liniambia pia kuwa amewahi kupewa pesa akawa nae pamoja usiku mmoja kipindi cha nyuma ila hawakua wapenzi.
Baada ya kama mwaka hivi, nilikua nimesikia mambo mengi sana kuhusu yeye, na ilionekana ni kweli yupo hivyo hata akisimama mbele ya macho yangu.
Hii haikua tatizo kwangu, lakini tatizo langu lilianza kuwa ni ukaribu wake na mume wangu, maana wanasema ndege wanaofanana huruka pamoja.
Nilipomaliza kuchunguza marafiki wa mume na kukuta yupo hivyo, nikajikuta nimeingiwa na mashaka na mume wangu pia. Hali hii ilikua kama utani ilipoanza, lakini baada ya muda ikawa ni tatizo hata kwangu, maana nilikua nakosa amani. Nilishindwa kumuamini moja kwa moja hata akisema anaenda kazini.
Kiufupi, nilikua najiona kama na mimi nasalitiwa na mwanaume wangu, kwa sababu niliona jinsi rafiki zake wanavyochezea wanawake huku wakiwa nao. Nilijikuta nipo kwenye ndoa ambayo sikujiona kama niko salama kabisa. Moyo wangu ulikua unawasiwasi sana, na huo wasiwasi niliufanya siri. Ndoa yangu ilikua kama inapita KWENYE KAGIZA.
Huo wasiwasi niliokua nao ulianza kunisukuma kufanya mambo ya ajabu kwa mme wangu. Yaani nilikua kila mara namfuatilia kama namchunga, halafu akifanya jambo nisilolielewa namtukana sana kuwa anawanawake nje ya ndoa.
Mme wangu alikua anakataa, ila nilikua namtupia maneno mengi sana hata akichelewa kurudi nyumbani kidogo tu.
Ilikua ni kawaida sana kumwambia “Rudi kwa wanawake zako, kalale huko huko!!! Mbwa wewe.”
Mwanaume wangu alikua ananiangalia na kunionya kuhusu maneno yangu, japokuwa alikua ananiacha niongee mpaka hasira ziishe.
Nilijaribu kuchunguza sana kama na yeye ana tabia hizo, lakini sikupata ushahidi wowote. Mwisho nikaamua kupanga siku ya kumuuliza mme yangu juu ya tabia mbaya za rafiki Mambe, maana yeye huongelea tabia nzuri tu.
Siku moja katika stori za hapa na pale tukiwa chumbani, nikaingizia hizo habari za rafiki yake. Nilishangaa kuona na yeye anakubali kuwa rafiki yake anafanya mambo hayo hapo mjini.
Ikabidi nimuulize, “Sasa kama rafiki yako yupo hivyo, inamaanisha na wewe upo hivyo?”
Akanijibu, “Hapana, mimi huwa namshauri aoe na kuwa na mwanamke mmoja.”
Pia alisema kuwa wanaume wanaweza kuwa marafiki sana lakini wakawa na tabia tofauti kwa wanawake. Mwanaume mmoja anaweza kumtesa mke wake lakini rafiki zake hawatesi wake zao. Hivyo nisiwe na wasiwasi.
Kiukweli moyo wangu haukuwa na chochote zaidi ya kumuamini, maana ushahidi wa yeye kunisaliti nilikua sina kabisa. Lakini nilijifunza kutochunguza sana marafiki wa mwanaume, maana walinifanya niwaze sana na kukosa amani kwenye ndoa yangu.
Unaweza kujikuta unaumiza moyo wako na kumhukumu mpenzi wako kwa sababu ya kuwachunguza rafiki zake….
Baada ya muda mingi kupitia walianza kutengana maana naskia tabia ya Rafiki yake ilizidi kuwa mbaya mpaka akawa anafumaniwa na wake za watu. Hii ilimfanya mme wangu kuwa mbali nae maana ananipenda sana. Alianza kunikataza mpaka mazoea nae.
Yote kwangu yalikua ni furaha maana nilipata amani ya moyo.
MWISHO
