Tulikua tupo mimi na rafiki yangu Samsoni kwenye chumba chetu tunacholala ambacho watu huita Geto. Ilikua mida ya kama saa moja au mbili usiku hivi alafu muda huo rafiki yangu alikua ananihadithia mechi ya mpira ambayo imetoka kumalizika saa 2 zilizo pita na sikwenda kuiangalia kwenye vibanda vya mpira siku hiyo kutokana na mawazo. Mawazo yalifanya kichwa changu kiwe vibaya sana muda huo kiasi kwamba nilikua naonekana kumsikiliza Samsoni lakini kiukweli nilikua hata simuelewi japo nilikua nacheka kila akicheka na kuitikia “Ebwana ee” ili asigundue kua akili yangu haipo kabisa kwenye anayonisimilia.
Katikati ya hadithi zake za mpira tukasikia simu imeanza kuita katika kisehemu tunachozichaji simu kilichokua pembeni kidogo ya dirisha la chumba hicho. Simu yangu na ya Rafiki yangu Samsoni, zote zilikua zipo chaji alafu simu yangu niliichomeka chaji ikiwa imezimwa. Hivyo simu iliokua ikiita muda huo ilikua ni ya rafiki yangu na tuliigeukia wote ilipokua inaita maana ilitushtua kwa kupiga kelele katikati ya maongezi. Baada ya hapo Samsoni alinyanyuka huku akijisemesha “Sijui nani huyu… itakua watu wa mpira hawa” alafu akaenda kuichukua ile simu mimi nikiwa namuangalia tu. Alipoishika simu na kusoma jina, nilimsikia akasema “Ah wewe Mpenzi wako huyu ananipiga huku. Sijui umekifanya nini tena kitoto cha watu”
Mimi nikashtuka kidogo alafu nikamuuliza “Ni Sabrina?” Samsoni alijibu “Ndio” alafu akasema tena “Ngoja nipokee nimsikilize” huku akiipokea simu na kuiweka sikioni. Mimi muda huo nilitaka nimwambie asipoke ila alikua ameishapokea kabla hata sijanyanyua mdomo kumwambia. Baada ya Samsoni kupokea simu, nilimsikia akisema “Halo Dada… niambie” alafu nikasikia kisauti kidogo cha Sabrina akasema “mambo vipi?” Samsoni akaitikia “kama kawa, vipi huko?” Sabrina akasema “safi. Mbona rafiki yako hapatikani kwenye simu? Upo nae hapo?”. Mimi kusikia hivyo nikashtuka, nikamwambia kwa ishara rafiki yangu Samsoni asiseme yupo na mimi.
Samsoni alinielewa akamjibu “Sipo nae. mimi niko mbali kidogo muda huu”. Sabrina alipoambiwa hivyo, akasema “Sawa, ukionana nae mwambie namtafuta” Samsoni akajibu “sawa” kisha simu ikakatwa. Baada ya hapo rafiki yangu alirudisha simu kwenye chaji huku akisema “Haya si umesikia? Eti anakutafuta. Sauti yake tu inaonekana mmezinguana nyie. Huu ugomvi siingilii” mimi nikacheka kwanza kidogo alafu nikasema “nitamcheki baadae”.
Baada ya hapo Samsoni aliniaga kuwa anatoka kidogo hivyo mimi nilibaki mule ndani nikiwa nimetulia tu ila kichwani kwangu mawazo ni mengi sana. Wakati akiondoka alisema pia “Alafu nilipokua anaangalia mpira, Tino alinipigia akaniambia amekutafuta hakupati hivyo umpigie” mimi nikaitikia “Ah sawa”.
Nilipokua pekeangu mule ndani, Mawazo yalinituma ninyanyue godolo tunalolatila maana Samsoni alikua anatabia ya kuweka pesa huko. Nilipofanya hivyo, nilizikuata pesa zake nyingi kiasi na nikazichukua maana niliona kama zinaweza nisaidia katika hali niliokuanayo kwenye wakati huo. Nilikua ni kama na muibia Rafiki yangu kabisa ili tu niweze kukimbia tatizo linalonipa Mawazo.
Mawazo niliokuanayo siku hiyo yalikua yamesababishwa na matokeo ya mimi kuanza kuzifungua kurasa za mapenzi katika maisha yangu. Nakumbuka miaka michache iliopita kambla ya siku hiyo nilikua nasoma sekondari kidato cha tatu na nilikua nasoma shule za kutokea nyumbani.
Tangu nilipoanza sekondari nilikua sijawahi jihusisha au kuwaza kuwa na mpenzi shuleni japo nilikua natamani. Hii ilikua ni kutokana na mambo mengi ikiwemo sheria za shule zilizokua zikikumbushwa kila siku na walimu. Na pia nilikua nawaogopa wazazi wangu kuniona nimejiingiza kwenye maswala ya mapenzi. Mbali na hayo, nilikua naogopa sana jinsia tofauti. Kuwasogelea na kuongea nao kulikua ni mthihani mkubwa sana kwangu kipindi hicho, hasa akiwa ananivutia.
Kwenye mambo ya kufanya vizuri shuleni kwa bahati mbaya nilikua siko sana huko. Uwezo wangu katika madaftari na mithihani ulikua wa kawaida sana. Nakumbuka darasani nilikua nakaa viti vya nyuma sana. Huko nyuma nilikua nakaa na rafiki zangu wawili ambao mmoja wapo ndio huyo anaitwa Samsoni, alafu kuna mwingine alikua anaitwa Tino. Kwaiyo tulikua kama tuna kikundi cha watu watatu nyuma ya Darasa. Darasa letu lilikua lina viti vinavyo ruhusu kukaa wawili na kiti nilichokua na kaa mimi, tulikua tunakaa mimi na Samsoni ila mwalimu akitoka tu, Tino alikua anakuja kwenye kiti kile, tunajibana watatu, tunapiga stori. Tino alikua anakaa kiti cha pembeni yetu ambacho kilikua karibu sana na sisi.
Tino alikua ni mwenzetu ila mambo yake yalikua mengi mno. Alikua ni msumbufu sana kiasi kwamba kila mtu alikua anamjua kwa usumbufu wake hapo shuleni. Watu walianza kumjua baada ya kuletwa na mzazi wake shuleni na kupigwa kutokana na kutolala kwao pamoja na kutokuja shule kwa siku 5 mfululizo katika kidato cha kwanza.
Tulikua tuna shirikiana sana Tino lakini usumbufu wangu haukufikia usumbufu wa Tino. Samsoni nae alikua kama mimi tu, hakumfikia usumbufu Tino hata kidogo. Ila katika mambo ya kwenye vitabu, wote tulikua hatufanyi vizuri sana japo hatui wamwisho Darasani.
Kuna siku asubuhi tulikua watatu Darasani kule nyuma ya Darasa tunapiga stori kwa kujiachia lakini ghafla akaingia mwalimu. Alivyoingia tu, tukafunga midomo alafu kila mtu kati yetu alikaa vizuri anapokaaga kisha watu wote darasani tukasimama kumsalimia Mwalimu. Baada ya kumsalimia, akaturuhusu tukae alafu nikakuta tu anasema “Nyie watatu uko nyuma hebu simameni”. Mh alivyosema hivyo nikawa nawaza “Anaongelea mimi na rafiki zangu au? Mbona anaangalia huku nyuma?” wakati najiuliza nikakuta mwalimu anasema tena “Nyie muliokua mnapiga kelele mpaka darasa zima mnasikika nyie huko nyuma simameni kabla sijawafuata.” Basi mimi nikaona huenda anatuongelea sisi, nikasimama na bada ya mimi kusimama, nikakuta na Rafiki zangu wawili wanasimama.
Baada ya hapo mwalimu akaanza kufoka “Hivi nyie mna matatizo gani? Inamana hapa shuleni mmekuja kupiga makelele au?” baada ya kusema hayo akaninyoshea mkono na kusema “Wewe hapo wewe inaonekana msumbufu maana hata Nywele haujanyoa. Hizo nywele ni siku ya ngapi nakwambia sitaki kuziona? Hebu sogea hapa mbele” mimi nikiwa mnyonge sana nilisogea taratibu pale mbele ya Darasa. Mwalimu aliniuliza “Unataka ni kupige ndio uanze unijibu?” mimi nikiwa naogopa sana nikamjibu “Hapana, samahani mwalimu nilitaka kunyoa jana ila umeme walikata”. Baada ya kumjibu mwalimu alifikilia alafu akasema “Kesho nisione hizo nywele, sawa!?” nikamjibu “Sawa” alafu nikakuta ananiambia “Na kule nyuma unakokaa, uhame. Kabebe madaftari yako kule nyuma uyalete hapa mbele kwenye hiki kiti ambacho hakina mtu”.
Baada ya mwalimu kusema hivyo nilishtuka maana nilikua sijazoea kukaa viti vya mbele ya Darasa, nikamwambia “Mwalimu hapo wanakaa watu wawili, itakua wameitwa nje”. Mwalimu akasema “Hatakama wakija hao wanao kaa hapa, waambie mimi ndio nimekuweka hapa. Kwanzia leo utakua unakaa hapa mbele. Nawakija hao, waambie wachukue kiti kingine wakae sehemu nyingine ila sio hapa”. Dah nilikua mnyonge sana siku hiyo, nikachukua vitu vyangu nyuma ya Darasa na kuhamia mbele ya darasa huku mwalimu akiniangalia.

Baada ya kukaa mbele mwalimu alianza kufundisha somo lake maana ndio ulikua muda wake huo. Mimi pele mbele nilikua sina amani kabisa maana sijazoea kukaa hapo alafu mbali na hilo, Daftari la mwalimu huyo nilikua sina. Lakini mwalimu alipoanza kufundisha nilichukua kidaftari flani cha ajabu, nikakiweka pale mbele ili kuzuga.
Nakumbuka baada ya kama dakika 10 hivi Mwalimu alipoanza kufundisha, alikuja mwalimu Mkuu akiwa ameambatana na wanafunzi kama watano hivi na mwanafunzi wa kike alikua mmoja. Darasa zima tulijikuta tunavutiwa kumuangalia yule mwanafuzi wa kike. Mwalimu mkuu alianza mazungumzo na Mwalimu aliekua Darasani na mazungumzo yao yalikua ni kwamba hao wanafunzi watano ni wageni na kwanzia siku hiyo watakua wanasoma humo Darasani. Walimu walipomaliza kuzungumza, wale wanafunzi wakaingia ndani ya Darasa alafu yule Mwalimu aliekua Darasani akawaambia watafute nafasi za kukaa mule Darasani. Kabla hata hawajapiga hatua sana, nikakuta mwalimu ghafla anamwambia yule mwanafuzi mgeni wa kike “Wewe usiende huko. Kaa hapa na huyu”. Mimi moyo ulishtuka sana maana alikua anamuelekeza yule Mwanafunzi wa kike akae na mimi kwenye kiti kimoja. Kiukweli mimi nilikua naogopa kukaa na jinsia tofauti hasa wakiwa wazuri ndio napoteza uhuru kabisa yani. Na Mwalimu alikua anamzingatia yule mwanafuzi wa kike kwa kiasi flani, kama ni ndugu yake hivi.
Nakumbuka yule mwanafunzi alikaa na mimi pele huku akiwa na viaibu aibu vya ugeni alafu na mimi wakati huo nina viaibu vya kumuogopa. Tukiwa tumekaa pale mwalimu aliwauliza jina wageni wote waliokuja na nilisikia yule Mwanafunzi wa kike akijitambulisha kuwa anaitwa Zuwena. Basi baada ya hapo mwalimu aliendelea kufundisha na mimi nikawa kama namsikiliza hivi ingawa akili yangu ilikua inahama. Yani nikua nikitupa jicho langu mara moja moja kwa yule Mwanafuzi wa kike kumuangalia jinsi alivyo. Japo nilikua naogopa, ila alikua anavutia sana kumuangali alafu alikua msafi sana. Kuna muda nilimtupia macho tukagongananae alafu akaona viaibu. Mimi nilipogongananae macho nilishtuka na nikaingiwa na woga zaidi ila woga ulipungua nipowaza “ Inamaana na yeye ananiogopa huyu. Dah ila mzuri mpaka raha. Ingawa naogopa ila hapa nijitahidi niwe hata rafiki yake tu. Sina hata rafiki wakike ujue”. Nakumbuka niliwaza mambo mengi sana kuhusu huyo mgeni bila kujua kuwa ndio namuingiza moyoni hivyo mtoto wa watu.
Baadae, mwisho wa kipindi cha mwalimu aliekua akifundisha ulifika na mwalimu alituachia maswali ya kufanya nyumbani tuyaandike alafu akasema anaondoka. Lakini kabla hajaondoka akasema “Nyie muliofika leo hakikisheni munaazima madaftari Kwa wenyeji ili muandike vitu vyote vya nyuma. Wewe Zuwena utachukua Daftari kwa huyo uliekaanae hapo, sawa!?”. Nikiwa pembeni ya Zuwena nikamsikia Zuwena akiitikia “Sawa” huku nikiwa nimeshtuka mno maana Daftari wanalo liongelea sina. Kichwani nikaanza kuwaza “Hapa mbona kama naenda kuumbuka kwa mgeni sasa. Huyu mwalimu na huyu mgeni wanajua Daftari ni hili lililopo Mezani lakini ukweli ni kwamba sina Daftari. Nikijieleza kwa huyu mgeni kuwa sina daftari, nitaonekana mjinga sana kwake na naweza shindwa kuwa rafiki yake. Dah tena anaonekana anaakili sana huyu, ntaumbuka leo.”
INAENDELEA…
4 thoughts on “MZIGO WA WAKUBWA 01 (Simulizi ya Kusoma)”