Moja kati ya simulizi ambayo huongelewa sana katika mifano ya maisha ni hii simulizi ya Mume, Mke, na Punda. Kama uijui vizuri simulizi hii, tulia uisome hapa chini;
Kulikuwa na mume na mke waliokuwa wakisafiri kijijini kwao wakiwa na punda. Njiani, walikutana na watu wa aina mbalimbali waliokuwa na maoni yao kuhusu safari yao.
Mume na mke walitembea kwa mguu huku wakiwa wamechukua punda wao akiwa amefungwa kwa kamba shingoni. Walionekana wamechoka, lakini walikuwa wakifurahia mazungumzo yao. Walipokutana na kundi la watu wa kijiji flani, walihisi macho yakiwatazama sana.
“Mna akili kweli? Mna punda lakini mnatembea kwa miguu! Kwa nini msimpande?” mmoja wa watu akasema huku akicheka.
Mume akatazama mke wake na akasema, “Labda wana ongea cha maana hawa. Hebu tubadilike.”
Mume alipanda punda huku mke akitembea pembeni. Baada ya muda, wakakutana na kundi jingine la watu.
“Angalia huyu mwanaume! Anawezaje kumpanda punda huku mke wake maskini anatembea? Hana hata huruma!” mmoja wa wanawake akasema kwa sauti ya lawama.
Mume aliona haya na kushuka. “Basi wewe panda sasa,” alimwambia mkewe.
Mke akapanda punda, alafu mume akaanza kutembea kwa miguu. Njiani, wakakutana na kundi jingine la watu waliokuwa wakifanya kazi shambani.
“Jamani! Angalia huyu mwanamke hana hata aibu. Anampanda punda huku mume wake mzee anatoka jasho akitembea!” mmoja wa wanaume akasema kwa dhihaka.
Mume na mke walitazamana na kuamua wote wapande punda.
Wote wawili walipanda punda na kuendelea na safari yao. Hawakufika mbali, wakaanza kusikia watu wakiwazungumzia tena.
“Hawa watu hawana huruma! Wote wawili wanampanda punda huyu mdogo. Wanataka kumuua kwa uzito wao?” mmoja wa wazee akasema huku akitikisa kichwa chake.
Mume na mke vichwa kikawaka moto, waliona bora wambebe huyo punda mgongoni ili wasisemewe tena. Wakafunga miguu ya punda kwa kamba vizuri na kumbeba kama mzingo. Walipokuwa wakivuka daraja, watu waliwaangalia kwa mshangao na kucheka sana.
“Jamani, angalia hawa wajinga! Wamegeuza mambo. Badala ya punda kuwabeba wao, wao ndio wanambeba punda!”
Kwa aibu, waliishiwa nguvu, punda akaanguka mtoni. Mume na mke wakakaa kimya huku wakitazama punda akizama majini…
Simulizi hii inamaana gani kwenye Maisha?
Simulizi hii inakumbusha kuwa katika Maisha, Haijalishi unafanya nini, watu watasema tu. Unaweza kufanya jambo kwasababu zako nzuri tu lakini wakaangaliwa kwa ubaya. Kiufupi, unapokua na ndoto au mambo mbalimbali unayotaka maishani, maneno ya watu usiruhusu yakuyumbishe au kukupoteza kama ilivyokua kwa wenye Punda.